Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt(as) -ABNA- Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia Masuala ya Kisheria na Kimataifa, Kazem Gharibabadi, ameikosoa vikali Australia kwa kile alichokitaja kuwa ni hatua za kuwawekea vikwazo vya kitaaluma madaktari wanaokosoa uhalifu unaodaiwa kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRNA, Gharibabadi aliandika katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X kwamba jaribio la kuwawekea madaktari marufuku au vikwazo vya kitaaluma kwa sababu ya kukosoa vitendo vya Israel ni shambulio dhidi ya uhuru wa kujieleza kitaaluma na dhamira ya taaluma ya udaktari.
Alisisitiza kuwa kuna tofauti kubwa kati ya kueneza chuki na kutetea watoto waliouawa pamoja na hospitali zilizoshambuliwa kwa mabomu, akionya dhidi ya kuchanganya masuala hayo mawili.
Gharibabadi alitoa wito wa kuheshimiwa kwa uhuru wa wataalamu wa afya kutoa maoni yao kuhusu masuala ya kibinadamu bila kukabiliwa na adhabu au vikwazo vya kitaaluma.
Your Comment